Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar

Mahakama ya Ardhi

Mahakama ya Ardhi Zanzibar imeanzishwa chini ya kifungu cha 3 (1) cha Sheria ya Mahakama ya Ardhi nambari 7 ya mwaka 1994 (S. 3 of the Land Tribunal Act no. 7 of 1994). Sheria hii ilitiwa saini mnamo tarehe 24/2/1995 na aliyekua Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa wakati huo MHE. DK. SALMIN AMOUR JUMA.

Madhumuni makubwa ya kuanzishwa sheria hii ni kuanzisha Mahakama ya Ardhi itakayokua inasikiliza na kutolea maamuzi migogoro ya ardhi kwa haraka na ikiwezekana kwa njia ya usuluhishi. Hivyo basi Mahakama za Ardhi zimechukua mamlaka ya kusikiliza mashauri ya ardhi yaliyokua yakisikilizwa na Mahakama za kawaida Unguja na Pemba, ambapo ilionekana kua, kesi hizo za ardhi zilikua zikichelewa sana kusiksilizwa na kutolewa maamuzi kiasi cha kuwepo malalamiko mengi kutoka kwa wananchi.

Sheria ya Mahkama ya Ardhi ya mwaka 1994, ilitambua, kuwepo kwa Hakimu mmoja tu wa kuhukumu kesi za ardhi Unguja na Pemba ambae aliitwa MWENYEKITI WA MAHAKAMA YA ARDHI.

Hali ya kuwepo kwa Hakimu (Mwenyekiti) mmoja tu wa kusikiliza na kutolea maamuzi mashauri ya ardhi Unguja na Pemba, pamoja na ongezeko kubwa la kesi kwenye Mahkama ya ardhi, kulisababisha kuchelewa kutatuliwa kwa mashauri ya ardhi. Kutokana na ucheleweshaji mkubwa wa utatuzi wa migogoro ya ardhi, ililazimu Serikali kuifanyia marekebisho Sheria ya Mahkama ya Ardhi mnamo mwaka 2008 kupitia Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mahakama ya Ardhi no. 1/2008 (The Land Tribunal Amendment Act No.1/2008).

Sheria hii ya marekebisho, iliruhusu kuanzishwa kwa Mahkama za Ardhi katika Mikoa yote ya Zanzibar. Aidha, iliruhusu kuwepo kwa Manaibu wenyeviti wawili wa Mahakama ambapo Naibu mmoja wa Mwenyekiti atafanya kazi Unguja na Naibu mwengine atafanya kazi Pemba. Pia Sheria hii, iliruhusu kuwepo kwa Mahakimu wa ardhi wa Mikoa kwenye Mahakama ya Ardhi mbali ya Mwenyekiti na Manaibu wenyeviti.

MAJUKUMU

Mahakama ya Ardhi ina mamlaka ya kupokea, kusikiliza na kutoa maamuzi juu ya migogoro inayohusu;-

  • Kesi zinazohusiana na madai ya haki ya matumizi ya ardhi na kushilikia ardhi yoyote ile.
  • Kusimamia uwekaji wa mipaka katika ardhi yenye shughuli ya ugawaji wa vikataa vya ardhi na suala jengine lolote ambalo linahitaji uwekeaji wa mipaka.
  • Kuthibitisha uhaulishaji au ukodishaji ambao umefanyiwa uchunguzi na Bodi ya uhaulishaji ya ardhi.
  • Umiliki wa ardhi katika maeneo ya miji na maeneo ya kilimo.
  • Kesi zinazoletwa na mkurugenzi wa ardhi kwa madhumuni ya kuirejesha ardhi yoyote inayomilikiwa na mtu yoyote.
  • Kurejesha Serikalini ardhi yoyote inayomilikiwa na umma.
  • Kuhaulisha mali ambapo ni kinyume na sheria zinazotumika na kilimo au viwanda vya mazao ya kilimo au mikataba ya ukodishaji wa ardhi.
  • Mabishano ugawaji usio wa kisheria na matumizi mengine yanayohusu migawanyo au ukataji wa vikataa vya ardhi usio wa halali.
  • Matumizi ya maendeleo ya ardhi kwa madhumuni ya hifadhi na matumizi ya mali asili.

KWA MAWASILIANO ZAIDI FIKA OFISINI KWAO MWANAKWEREKWE AU WASILIANA NAO:

P.O.BOX 811 ZANZIBAR, TANZANIA.

Tel: +255 242234154 

Website/Tovuti: www.landtribunalsmz.go.tz    

Email/Barua pepe: info@landtribunalsmz.go.tz